Dhana ya Wakati na Muundo Katika Riwaya za Kiswahili

Saa ya Ukutani

Swali

Kwa kutumia mifano toka riwaya teule mbili za waandishi wawili: Watoto wa Maman’tilie na Mfadhili, jadili dhana ya wakati na muundo wa riwaya.

Jibu:

Katika riwaya, dhana ya wakati humaanisha: mwaka ambao kitabu kimeandikwa na kuchapishwa, ndani ya kitabu, wahusika wanazungumzia matukio ya wakati gani na wasomaji wa riwaya waliisoma wakati gani.

Kwa upande mwingine, muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi. Katika riwaya, muundo hujishughulisha na idadi ya sura na mtiririko wa matukio. Mtiririko unaweza kuwa wa moja kwa moja au wa urejeshi.

Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie, imeandikwa na Emmanuel Mbogo. Riwaya hii inahusu maisha ya dhiki wanayopitia Watanzania. Katika hali ya kusikitisha, kwa sababu ya kukosa pesa, watoto wanafukuzwa shule na kujikuta wakijiingiza katika tabia hatarishi ikiwemo uuzaji wa mihadarati.

Nayo riwaya ya Mfadhili, imeandikwa na mwandishi Hussein Issa Tuwa. Riwaya hii inahusu kisa cha ajabu sana cha bwana mmoja aliyeamua kumpatia kipande cha ini mwanamke ambaye alimfanyia usaliti ulioumiza hisia zake kwa viwango vya juu. Ama jina la kitabu hiki, Mfadhili, inahusu ufadhili uliofanywa na bwana huyu-Gadi Bulla.

Kwa kutumia mifano kutoka riwaya hizi mbili: Watoto wa Maman’tilie na Mfadhili, dhana ya wakati na muundo imeweza kujadiliwa.

Kwa kuanza na Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie, dhana ya wakati na muundo inajadiliwa:

Katika dhana ya wakati, riwaya ya Watoto wa Maman’tilie imeandikwa na kuchapishwa mnamo mwaka 2002. Mchapishaji wa riwaya hii ni kampuni ya Heko Publishers iliyoko katika jiji la Dar es Salaam.

Ndani ya riwaya ya Watoto wa Maman’tilie, yanazungumzwa matukio yaliyojiri mwaka 2002 kurudi miaka ya nyuma zaidi. Kwa mazingira, inaonekana mwandishi aliandika kitabu chake kabla ya mwaka 2002, hivyo upo uwezekano, kitabu hiki alikiandika mwaka 1999, 2000 au 2001. Katika wakati huu, wanafunzi wa shule ya msingi walilazimika kulipa ada. Ama sivyo, walifukuzwa shule. Ni mwaka 2001 ndipo ada katika shule za msingi ilipofutwa na wanafunzi kuanza kupata elimu ya msingi bure.

Katika upande wa muundo, riwaya ya Watoto wa Mamantilie, imetumia muundo wa Urejeshi. Mwandishi amemuonyesha Lomolomo akiwa katika hali ya ulevi, baadaye anatukumbusha alipokuwa anafanya kazi bandarini. Vilevile anawaonyesha Kurwa na Doto wakiishi peke yao. Lakini baadaye anatukumbusha kipindi walipokuwa wanalelewa na mama yao ambaye hata hivyo alifariki kisha wakalelewa na Jane ambaye naye anafariki.

Pia, riwaya hii imebeba jumla ya sura tano. Sura ya kwanza inaonyesha watoto wasio na ada wala sare wakifukuzwa. Sura ya pili, Peter anaanza tabia ya kwenda jaani kutafuta chochote ili auze apate pesa za kurudi shule, sura ya tatu inaongeza simanzi kwa kuonyesha kuwa, watoto Zita na Peter bado hawakuwa wamerudi shule kwani, hali ya kiuchumi ya mama ilikuwa mbaya mno, sura ya nne, watoto hawajarudi shule, Maman’tilie amesafiri na sasa watoto wanafanya kazi ya kuuza genge, sura ya tano, inaisha kwa kuonesha mtoto Zita akifariki kwa kichaa cha mbwa, Peter anakamatwa kwa kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya na Lomolomo anapoteza maisha kwa kuzidisha kiasi cha pombe.

Sambamba na hayo, riwaya ya Mfadhili, nayo ina dhana ya wakati na muundo kama inavyojadiliwa:

Kwa kuanza na dhana ya wakati, riwaya ya Mfadhili imeandikwa mnamo mwaka 2007, ikachapishwa na Macmillan Aidan yenye makazi yake katika Jiji la Dar es Salaam. Riwaya hii ilipatikana pale yalipoendeshwa mashindano ya uandishi wa riwaya, ndipo Issa Tuwa akaibuka kidedea na riwaya hii kuchapwa hatimaye kupata umaarufu sana.

Ndani ya riwaya hii ya Mfadhili, yanazungumziwa matukio yaliyotokea katika Tanzania mpya. Tanzania ya utandawazi tena inayopenda sana kusoma hadithi na visa vya mapenzi. Matukio ya kazi, ulevi, usafiri wa ndege na matibabu ya kisasa kama upandikizaji wa ini, yanazijadili vyema zama mpya za sayansi na teknolojia.

Kwa upande wa muundo, riwaya hii imetumia muundo wa urejeshi. Sura ya kwanza wanaonekana Nunu na Boaz wakimtafuta Gaddi Bullah. Sura zinazofuata, zinaeleza maisha na mikasa ya Gaddi, kwa nini alitoweka na maisha yake ya nyuma. Riwaya hii inakuwa na mwisho mbaya, kwani Gadi Bullah anapoteza maisha kwa sababu ya ufadhili aliofanya.

Pia, riwaya hii ina jumla ya sura zipatazo kumi. Sura ya kwanza Nunu na Boazi wakimtafuta Gaddi Bullah bila mafanikio na hatimaye kumteka dada yake [Bi. Hanuna] na kumpeleka hadi nyumbani kwa akina Dania. [Uk. 1-56]. Sura ya pili hadi ya nane Mwandishi anaanza mwanzo, hapa tunaona kukutana kwa Gaddi Bullah na Nyambuja na kuoana, Gaddi kusalitiwa na huyo mke wake, kuvunja ndoa yake, Kuhamishiwa Dar es Salaam, kukutana na Dania na kuanza uhusiano wa kimapenzi na kusalitiwa na Dania na hatimaye Gaddi Bullah kutoweka. [Uk 57-128] Sura ya tisa hadi ya kumi Dania anaanza kuumwa ini, Dania anakimbiwa na Jerry kwa mara ya pili, Dania anaandika barua akimuomba Nunu aipeleke kwa Gaddi Bullah, Gaddi anajitolea ini kumfadhili Dania, Gaddi anaanza kuumwa, Dokta Virani anatoa siri juu ya mfadhiri wa Dania, Gaddi anafariki dunia na ndio mwisho wa riyawa hii. [Uk 129-148].

Kwa kuhitimisha, riwaya huwa na dhana ya wakati na muundo. Katika riwaya hizo mbili, zote zinafanana katika wakati ambao zimeandikwa. Riwaya hizo, zote ni matokeo ya miaka ya 2000 na hazijaenda mbali na wakati huo. Riwaya ya Watoto wa Maman’tilie ikijikita katika kuuzungumzia umasikini uliokithiri, umasikini unaofanya watu walale njaa, wengine wajiingize katika ujambazi na wengine wakose hata shilingi chache za kusomeshea watoto wao elimu ya msingi. Riwaya ya Mfadhili nayo imejikita katika mambo haya haya ya kizazi kipya. Mapenzi kupita kiasi na visa vyake. Kuumizwa moyo kwa kumfumania mke, kupata mwanamke mwingine lakini bado akakuacha, akaugua na kurudi kwako kuomba msamaha, unampa kipande cha ini ili apone maradhi, lakini inakusababishia kifo chako, ni miongoni mwa kazi nyingi mno za miaka hii ambazo kusema kweli zimejikita katika masuala ya mapenzi na hazionyeshi kujali sana upande wa jamii na siasa ambao umeonekana kuwa hauna soko.

Marejeo:

Mbogo, E. (2012). Watoto wa Maman’tilie. Dar es Salaam: Heko Publishers.

Tuwa, H. (2007). Mfadhili. Dar es Salaam: Macmillan Aidan.

https://www.mwalimumakoba.co.tz/2017/05/uhakiki-wa-kazi-za-fasihi-andishi.html

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024

Vichekesho vya Kuchekesha na Kuvunja Mbavu 1