Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya 10
“Nkuu wa Nkoa kaja kwa ku shtukiza… patachimbika humu
ndani nakwambia, atatumbuliwa ntu baada ya ntu,” alisema bibi mwingine
aliyekuwa anamuuguza mjukuu wake.
“Unapiga simu wapi?” nilimfokea nesi ambaye alionekana
kupiga simu kuwaita wakubwa wake. “Usipige simu, usimuite yeyote, hapa nimekuja
kwa kushtukiza na nitaingia kila wodi kwa kushtukiza.”
“Sawa mkuu,” walijibu watumishi wale wa afya. Wagonjwa
wakatabasamu.
“Sasa sikiliza,” niliendelea. “Wagonjwa watibiwe, pesa
italipwa baada ya matibabu, tuhakikishe tunaokoa uhai kwa gharama yoyote. Pesa
zipo tu na haziwezi kamwe kufanana na thamani ya uhai wa mwanadamu.”
“Ndiyo mkuu,” walijibu.
“Natoka humu katika ziara yangu hii ya kushtukiza,
msipige makelele wala msinifuate, pia msipigiane simu, nakwenda kwenye jengo
lile wodi ya wazazi, nawatakia utekelezaji mwema.”
Nilitoka katika wodi ile na kuanza kuelekea wodi ya
wazazi. Nilikuwa na hofu kwamba, watu wangeongezeka zaidi, lazima ningegundulika
kuwa mimi siyo mkuu wa mkoa. Hii ingekuwa kesi kubwa tena ya aibu. Vilevile
sikuwa nimepanga kuwa nitambulike hivyo, ni watu niliowakuta wodini ndiyo
walinipachika cheo hicho.
Nilitembea haraka nikazipandisha ngazi za jengo la wodi
ya wazazi. Nilikuwa napiga jicho nyuma kwa kuibia, kumbe maelekezo yangu
hayakufuatwa, kuna manesi walishapiga simu na nyuma kiasi cha hatua mia mbili,
niliona watu wengi wakija nilipo, niliweza kuwatambua watu hao, mmoja wao
alikuwa Daktari mkuu wa hospitali hiyo. Alikuwa anakuja nilipo akiongozana na
madaktari wengine watano na askari watatu.
Sasa niliiona hatari iliyokuwa inaninyemelea. Daktari
mkuu na wenzake wote wasingeshindwa kutambua kuwa mimi sikuwa mkuu wa mkoa hata
kama mkuu mpya wa mkoa hakuwa ameanza kuonekana katika Luninga. Wazee hawa
wanawafahamu viongozi wote kwani ni jamaa zao.
Nilitembea haraka nikalifikia jengo la wazazi na sasa
nilikuwa ndani ya jengo hilo lililo juu kimo cha ghorofa moja. Niliwaacha mbali
watu wale lakini nao walikuwa wakija kwa kasi zaidi. Niliingia wodini kama
ninaye salimia watu. Jengo hili lina upande wa kushoto na kulia, mimi
nilielekea kulia, nikatembea mpaka mwisho na bahati njema, mapokezi hapakuwa na
daktari wala nesi na wodi nzima ilikuwa na mgojwa mmoja tu aliyekuwa anaongezwa
damu na alilala usingizi.
Nilifungua dirisha kubwa la vioo kisha nikatoka kwa
kushuka taratibu, nilipoona kimo cha chini ni kidogo, nilijitupa kikomandoo,
kisha kwa kuinama, nikakimbia mpaka ulipo ukuta, nikauparamia kama mjusi na
kuukwea mpaka kilele chake, halafu ‘puuu’, nilikuwa nje ya hospitali. Huko
nyuma sikujali kama kuna mtu aliniona au hakuniona.
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya 11