Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Nane

Kidume usiku wa manane

Silaha niliyokuwa nayo, Beretta, iligunduliwa na mtaalamu Bartolomeo Beretta mwaka 1526 huko Gardone Val Trompia nchini Italia. Ni silaha nzuri ya kawaida ambayo imekuwa ikitumiwa na watu binafsi kwa kujilinda.

Kama alivyo mtaalamu Bartolomeo Beretta, nami mtaalamu Mako, niligundua silaha kubwa ya maangamizi niliyoipachika jina Mako 29. Ikiwa na maana kwamba, Mako aligundua silaha hiyo akiwa kijana wa miaka 29 tu.

Mako 29, ina uwezo wa kupiga risasi 3,000 kwa dakika na inaweza kumdhuru adui akiwa umbali wa hata kilomita mbili. Ukichunguza kwa makini utagundua Mako 29, imeishinda AK 47 ya Warusi na M16 ya Wamarekani karibu mara tatu au tano, pengine hata kumi hesabu zikifanywa vyema. Silaha hiyo tayari ilikuwa mikononi mwa jeshi letu, na walikuwa wanaifanyia mazoezi ili ianze kutumika. Hata hivyo, kwa sababu mimi ndiyo mbunifu wake, nilikuwa nayo moja niliyoificha kwa siri. Na hata ningetaka, ningetengeneza nyingine. Mpishi hafi kwa njaa.

Ni kama utani, lakini zilikatika wiki tatu bila kumuona Asi wala kupata fununu zozote zenye msaada zaidi ya zile taarifa za Iki. Sikukata tamaa, niliendelea kutembeatembea nikiwa na matumaini ya kuona chochote chenye msaada wa kumpata.

Kwanza utajiuliza Asi siyo ndugu yangu, lakini namtafuta sana kwa nini? Hata nikijibu namtafuta kwa sababu ya zile pesa, shilingi elfu kumi na tisa za Kitanzania bado italeta mashaka. Vipi nikisema nilianza kumpenda msichana huyo halafu nikaongeza hoja kwa kusema, kulinda watu wasipotee wala kunyanyaswa ni jukumu langu, nisiongee sana. Wengine sisi, kazi zetu huwa hazisemwisemwi.

Mtembea bure si sawa na mkaa bure. Siku moja saa nne usiku niliamua kutoka niende matembezini. Nilipita katika geti nikakata kulia kama askari. Nikafuata njia nikikunja kona hii na ile mpaka nilipokuwa katika njia fulani ambayo pembeni kushoto kuna zahanati ya Kambangwa na kulia kuna hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala. Nilitembea nikavuka barabara, kisha nikanyoosha na kuingia katika danguro.

Katika danguro hilo, wanawake walijiuza kila mmoja akiwa kakaa katika mlango wa chumba chake, na kama ungevutiwa naye, ungeingia ndani naye angekufuata. Malipo hayakuwa makubwa, shilingi elfu tatu zingetosha kukupatia huduma.

Kwa hivyo, lilikuwa jengo lenye vyumba vingi, lililowekwa njia upande huu na ule ili watu wapite kujionea biashara hiyo ya nyama. Mimi sikupita hapo kununua, tutunze afya zetu tafadhali. Nilipita hapo kusafisha macho, na pengine labda ningemuona mtu niliyemtafuta.

Wakati nikiendelea kutembea katika danguro lile, niliona wateja wakiingia na kutoka, bila shaka wameridhishwa na huduma. Wanawake ambao hawakuwa na wateja, walinitazama kwa uchu tena kwa kunitamanisha haswaa.

Lakini sikuwa na bahati, nikikaribia kulitoka danguro hilo, askari walivamia na kutuamrisha wote tukae chini. Sasa nikawaza kosa langu nini, ukahaba au kupita njia ile?

Askari walituchukua wanaume wakitufunga mashati wawiliwawili mpaka kwenye gari lao kubwa. Nakadiria tulikuwa wanaume ishirini, wenzangu wote walikamatwa wakiwa kwenye vyumba vya makahaba au wakiwa wametoka kupata huduma au wakivizia huduma. Ni mimi pekee niliyekamatwa kwa sababu ya kupita pale, sikuwa na mpango wowote na watu wale zaidi ya kusafisha macho na kumtafuta Asi.

Jambo moja lilinishangaza, japo tulikamatwa katika danguro, ni wanaume tu ndiyo tuliwekwa kwenye gari. Wanawake wale waliokuwa wakiifanya biashara ya ukahaba, hakukamatwa hata mmoja, na kuna baadhi ya askari niliwaona wanafunga zipu zao baada ya kutoka kwenye danguro. Nikashangaa tu!

“Aloo polisi kanitoa nimeshalipia, kaingia yeye kula zigo,” alilalamika mtuhumiwa mwenzetu mmoja aliyekuwa upande wa mlango wa gari kubwa la polisi. Mimi nikashangaa tu!

Wakati tupo kwenye lile gari, askari wawili walikuwa wanatulinda, baadae wakarudi wenzao wawili, wakabadilishana, waliotulinda mwanzo wakakimbia kuelekea kwenye danguro, walipotoka, walikuwa wanafunga zipu zao. Nikashangaa tena!

Tukiwa kwenye gari tulishtushwa na sauti ya afande, “Nyie wachinga… Kila mmoja atoe elfu thelathini aachiwe au twende kituoni.”

Watuhumiwa wenzangu wapatao kumi na tano walitoa kiasi hicho cha fedha. Watano walipiga simu kwa jamaa zao wakatumiwa, wakasindikizwa na askari Tumbotumbo kwenda kwa wakala kutoa fedha hizo na huko wakaachiwa. Sasa tulibaki wawili, mimi na jamaa mmoja ambaye baadae niligundua anaitwa Chafu Tatu.

Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Tisa

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024