Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Nne
Katika kumbukumbu nzuri, nakumbuka kwenda Coco Beach na
Asi, huko tulikula mihogo ya kuchoma, tukaogelea na kuzungumza mengi.
“Bwana Mako,” Asi aliniita.
“Naam,” niliitika.
“Uliwezaje kuwadhibiti wale wezi wa siku ile, tena wakiwa
na silaha?”
“Unajua…” nilisema nikitafakari namna ya kubadili
mazungumzo ili asinichimbe sana. “Katika Jiji hili la Dar es Salaam, kuna watu
wanajiona wao ni wababe mno na huwaambii chochote. Achana na huo mkasa,
nakumbuka siku moja nikitoka katika matembezi yangu, jamaa mmoja alisimama katikati
ya njia na kuniamrisha nitoe pesa.
“Jamaa yule wala hakuwa na silaha yoyote na alikuwa peke
yake. Nilimuuliza, Unajiamini nini kutaka kuniibia mimi tena ukiwa peke yako?
Jamaa akawa mkali na akaanza kusogea nilipokuwa. Alipofika hatua tatu ili aweze
kunifikia, nilimpiga ‘jebu’ moja iliyofuatiwa na ‘right’ akadondoka chini huku
analia, Umenipiga na jiwe, umenipiga na jiwe! Nilimsogelea alipodondoka na
kumuonyesha mikono yangu huku nikisema, “Siyo jiwe ni ngumi!”
Asi alicheka sana, sikutaraji kama simulizi ya mkasa wa
mapigano inaweza kumchekesha mtu. Msichana alicheka, nikaona kabisa mbavu
zinamuuma na almanusura adondoke na kiti kama isingekuwa kuwahi kukikamata.
Ni katika siku hiyo niligundua kuwa Asi alikuwa mgeni
katika Jiji la Dar es Salaam, binti huyu alitoka Tanga na alikuwa na jambo
fulani na Babuu. Hata hivyo, hakunieleza Babuu ni nani na alifuata nini hapa
mjini.
Tulikaa mpaka saa 12 jioni, tukaanza kurudi nyumbani kwa
mwendo wa kutembea polepole. Mimi kushoto, Asi kulia.
Tulichukua njia za ndanindani tukaibukia katika kanisa la
Mtakatifu Petro. Ni katika kanisa hili, Marehemu Rais John Pombe Magufuli,
alizungumza kwa mara ya mwisho kabla hajafikwa na mauti. Nakumbuka katika
hotuba yake alisema hajakataza watu kuvaa barakoa ili kujikinga na Ugonjwa wa
UVIKO-19, wengine wakiuita Korona. Ila alisisitiza kwamba, barakoa zingine ni
mbaya na tuwe makini.
Hakuishia hapo, alimpongeza paroko kwa kitendo chake cha
kutovaa barakoa, na alishangazwa na Masista wawili waliokuwa wamevaa barakoa.
Nakumbuka alisema, “Anayeilinda nafsi yake, ataipoteza.”
Yeye hakuvaa barakoa, na hakukataza watu kuvaa barakoa,
ila hakuziamini barakoa kutoka mataifa ya nje. Kuna mahali aliwapongeza sana
watu waliokuwa wamevaa barakoa za kushona wao wenyewe. Alisikika akisema, “Vita
ya uchumi ni mbaya.”
Alikuwa mzalendo kwelikweli aliyetamani taifa lake
lipende vyake. Ndiyo maana hata katika kupambana na gonjwa la Korona,
alihamasisha watu wajifukize.
Niliendelea kuuchapa mwendo na Asi, sasa tulivuka
barabara ya Ali Hassan Mwinyi, kushoto tukauona ubalozi wa Ufaransa.
“Unaona jengo lile?” nilimuuliza Asi aliyekuwa kanishika
mkono.
“Naliona,” msichana alijibu.
“Pale ndiyo gaidi Hamza aliwasumbua sana askari. Kile
kijengo kidogo cha pembeni kile cha kukaa mlinzi, alijificha humo na kuanza
kuwachachafya askari na ‘SMG’ mbili alizopora kwa askari haohao.”
“Walikufa askari wengi eeeh?”
“Sina uhakika, ila nakadiria walikufa watano.”
“Kwa nini Hamza aliamua kufanya hivyo?”
“Baada ya tukio, baadhi ya watu walisema alidhurumiwa
madini yake na askari hivyo alikuwa katika harakati za kulipa kisasi. Hata
hivyo, uchunguzi ulipotoka, vyombo vya sheria vilisema Hamza alikuwa kijana wa
hovyo tu na hakudhurumiwa chochote ila alikuwa mtu wa hovyo, gaidi. Vyombo vya
sheria vikasema tena na kuwaomba sana wazazi wasizae watoto wa hovyo kama
Hamza.”
“Utajuaje kama umezaa mtoto wa hovyo?” aliuliza Asi
akinitazama, mbele akapita muuza karanga, nikamsimamisha na kununua za shilingi
mia tano zikiwa zimewekwa katika kikaratasi, chache nikamimina katika kiganja
cha Asi, nyingi nikabaki nazo. Usinione mchoyo, baadae nilimuongeza.
“Mtoto wa hovyo…” nilikumbusha nikitafuna karanga. “Ni
ngumu kufahamu, lakini simlaumu aliyesema hivyo pengine zilikuwa ni hasira za
kupoteza askari wake. Laiti kama ningekuwepo siku hiyo, ningehesabu risasi
anazorusha Hamza, zingefika risasi sitini, basi ningebaini bunduki zake mbili
zimekwisha risasi, na hapo ndipo ningejitokeza mbele yake na kumkamata kama
kuku.”
Asi alinitazama, akatabasamu, halafu akajisogeza karibu yangu
zaidi, tukaendelea kutembea, tukitafuna na kuzungumza.
Mwisho tulivuka Barabara ya Kawawa. Tukakiona kituo cha
Mwendokasi cha Morocco. Mradi wa mwendo kasi ulilenga kupunguza kero ya
usafiri, lakini mimi sikuona upunguzaji wa kero hiyo. Niliishia kusikitika tu
kuona jinsi abiria wa Mbezi walivyojazana kwenye huo mwendokasi, wengine
walikosa pa kukanyaga wakiwa humohumo kwenye mwendokasi. Mtu pekee aliyekuwa
amekaa kwa huru mwendokasini humo, alikuwa ni dereva. Akina siye waliibiana,
wakauzidisha umasikini wao maradufu. Halafu kauli chafu za madereva, ati “We
mzee geuka kule shika bomba!” Kauli gani hizi? Kauli za kishwaini ushenzi.
Tuliukanyaga mdogomdogo nikiwa na kiumbe mdogo wa kike.
Tena, nilimsindikiza mpaka mitaa ya kwao na tuliagana, mimi nikarudi katika
makazi yangu ya muda. London Lodge.
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Tano