Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Tatu
Nilinyanyuka huku nazungumza, “Mheshimiwa, huyo dada hana
funguo ya kabati la fedha, mimi ni mfanyakazi mwenzake nakuja kukupatieni.”
Wakati nazungumza nilikuwa nasogea kuelekea walikosimama,
nilitembea mpaka karibu kabisa na yule jamaa mwenye silaha, nikiwa nimeukunja
mkono wa kushoto, huku nikichezesha mkono wa kulia wakati ninapozungumza,
nilimzubaisha yule jamaa mwenye silaha, nikampiga ngumi kali ya kidevu kwa
mkono wangu wa kulia na kabla hajadondoka chini, nikawahi kuikamata silaha
yake. Sasa ikawa yangu, yule mwenzake alibabaika, nikamwamuru akae chini
haraka.
Jamaa wale walifungwa kamba mpaka walipokuja askari
kuwakamata. Hakuna aliyeweza kuamini kuwa, mahali pale palitoka kufanyika tukio
la uvamizi wa silaha. Mziki uliendelea kama kawaida na watu walicheza kwa nguvu
zaidi kuliko mwanzo. Hata hivyo, watu walianza kuniangalia sana, wengine
wakinishukuru na kuninunulia vinywaji vya bure kwa ushujaa ambao nilionyesha.
Burudani iliendelea kutoka kwa ma Dj ambao nilitambua
walikuwa wawili na walifanya kubadilishana, muda huu alisimama mwingine,
mwembamba, kavaa kiatu cheusi kirefu na amenyoa kiduku. Nikasikia kionjo, “Auto
waharibiee.” Nikabaini bila ya mashaka yoyote kuwa, pale palikuwa na Dj Auto
Run.
Ulipigwa wimbo wa Amapiano, nikashangaa kuona Asi akiwa
na filimbi mdomoni, alipuliza filimbi yake kufuatisha filimbi ya kwenye wimbo, mbali
na kupiga filimbi, alicheza kwa maringo hata akawa kama kishada kilichokata
kamba.
Hata hivyo, burudani ilielekea ukingoni pale Asi
alipoomba arejee nyumbani kwani mida ile ingekuwa rahisi kwa Babuu kuamka.
Niliagana naye, nami sikukaa sana, nikaondoka kuelekea makazi yangu.
Mengi hayajulikani kuhusu mimi na sitaki kuyasema. Lakini
katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu sikwenda kukaa kwa muda mrefu, basi
niliishi katika Nyumba ya Wageni iliyoitwa London Lodge. Nyumba hii ya kulala
wageni ipo Kinondoni, pembezoni kabisa mwa mahakama ya Kinondoni, mahakama
nzuri ya kisasa, na ungetazama mbele ya geti la London, ungeiona shule ya
Sekondari Kambangwa.
Nilipewa chumba ambacho sikumbuki namba yake, ila
nakumbuka kilikuwa chumba kilichokaribiana sana na mapokezi. Vyumba vingine
vilivyokuwa mbele, vilipachikwa majina ya miji, japo sikumbuki vizuri, lakini
nadhani kipo chumba ambacho kiliitwa Spain.
Ndani ya chumba changu palikuwa na kitanda cha chuma
kilichokuwa na godoro laini, sofa la mtu mmoja jeusi na choo pamoja na bafu.
Huduma zote nilizotaka nilizipata, na niliwaomba wenyeji wangu kwa kuwa
nilikuwa mkazi wa siku nyingi, basi chumba changu kiheshimiwe, na asiingie mtu
yeyote kusafisha bali shughuli zote ningezifanya mimi, na niliwaomba, funguo
nitembee nayo muda wote ninapotoka. Walinielewa, maisha yangu yakawa mazuri
mno. Hata hivyo palikuwa na kero moja ambayo niliivumilia, dari lilionekana
kuoza na vumbi lake lilielekea kunisababishia mafua.
Maisha yangu katika nyumba hii ya wageni, kwa muda wa mwezi
mmoja tu niliokuwa nimekaa, nilishudia vioja vingi, lakini kikubwa zaidi ya
vyote, ilikuwa ni fumanizi. Jamaa mmoja alimfumania mke wake, lakini huyu bwana
aliyemfumania naye ni jamaa aliyekuwa akimdai. Basi alifoka sana na mwisho
alisikika akisema, “Mayombi, deni lako tumemalizana, hunidai tena!”
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Nne