Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Saba
Niliiingia na kuufunga mlango taratibu, kisha nikaanza
kutembea kwa tahadhari kubwa. Sikutaka kuwasha taa, kwanza sikufahamu vilipokaa
viwashio, nikatumia tochi yangu. Ilikuwa nyumba ya vyumba sita. Katikati
korido, pembeni kushoto vyumba vitatu na pembeni kulia vyumba vitatu.
Nikiwa nasogea, nilikwaruzwa na kitu mguuni, nikazima
tochi haraka halafu nikaganda kama sanamu, mkono ukiwa kiunoni nilipoipachika
Beretta. Baada ya sekunde tatu,
nikawasha tochi, nikaishia kumuona paka mkubwa, silaha ikarudi kiunoni, sikuwa
pale kupambana na nyau!
Vyumba vitano havikufungwa, nilivichunguza vyote, nikaona
dalili za watu kulala humo kwa kurundikana. Niliona magodoro chakavu yaliyopangwa
kivivu, ndoo nne za kuogea kwa kila chumba na vipande vya sabuni.
Baada ya kumalizana na vile vyumba vitano, sasa
nikakiendea kile chumba cha sita kilichokuwa kimefungwa. Nilitumia funguo
yangu, mlango ukafunguka. Tofauti na vile vyumba vingine vilivyokuwa na
magodoro machafu na mrundikano wa taka, hiki kilikuwa kizuri, tena kuna kitanda
kikubwa na chini pamesakafiwa kwa vigae vya kuteleza. Hata wewe tayari
umegundua kwamba, hiki ni chumba alichoishi Babuu.
Nilikichunguza lakini sikupata chochote cha maana. Zaidi
niliiishia kuona misokoto miwili ya bangi iliyokuwa imefichwa ndani ya mto wa
kulalia. Nilipangilia kila kitu vyema kisha nikaondoka kurejea katika makazi
yangu.
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Nane