Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya Sita
Nilifika katika nyumba ile, nikagonga mlango kwa dakika
nyingi bila kufunguliwa. Mlango ule ulikuwa mkubwa tena wenye pande mbili
zilizokutana katikati ambako palikuwa na kitasa. Baada ya gongagonga bila
majibu, nilijaribu kuzungusha kitasa, hapo nikagundua palifungwa. Sikuelewa
kama mwenye nyumba alikuwa ndani au alitoka, hayo ndiyo matatizo ya vitasa!
Hata hivyo nilihisi wenye nyumba hawakuwepo. Niliamua
kupeleleza kidogo kuhusu nyumba ile na wakazi wake, kwa kuwa sikutaka
kujulikana kama nilikuwa ninapeleleza, niliamua kutafuta watoto wadogo, hawa
wasingeweza kunitilia shaka lolote.
Niliingia katika chumba kimoja cha biashara kilichokuwa
kimeandikwa ‘play station’. Ndani yake mlikuwa na watoto waliokuwa wanacheza
michezo mbalimbali ya kompyuta. Nami nilikwenda moja kwa moja mpaka katika
sehemu moja iliyokuwa wazi, nikaomba niwekewe GTA, haraka nikawekewa na
nikaanza kucheza.
Haikuchukua hata dakika moja, watoto watano walikuwa
nyuma ya mgongo wangu wakitazama jinsi nilivyokimbizana na maaskari katika
mchezo ule wa GTA.
“Nani anaweza kunisaidia kuwakimbia hawa askari?”
niliuliza.
“Mimiiiiii!” watoto wote walijibu. “Wewe unaonekana
unajua sana, kaa hapa uendelee, halafu nyinyi wengine, mtakuwa mkipeana naye
zamu, nitalipia hela ya siku nzima leo mcheze tu mpaka mfike mwisho. Halafu
wewe rafiki yangu, hebu njoo hapa nje mara moja nataka nikutume kitu,” nilisema
nikimshika mkono mtoto mmoja, makadirio miaka tisa, ambaye alionekana mjanja
zaidi ya wengine.
Nilikaa katika kiti nje ya chumba kile cha michezo.
Niliyekaa naye tayari nilishamfahamu jina lake, aliitwa Iki.
“Iki, ile nyumba nani anakaa?” niliuliza nikinyooshea
kidole nyumba ambayo nilimuona Asi akiishi.
“Anayeishi hapo ni mgeni,” alijibu Iki akichungulia
wenzake walivyokuwa wakiifaidi GTA.
“Iki tukimaliza mazungumzo, nitakulipia sehemu ya peke
yako ucheze bila kupeana zamu na mtu. Haya endelea, anayeishi hapo ni mgeni,
eheee…”
“Kahamia juzi juzi tu.”
“Aliyekuwa anaishi hapo mwanzo ni nani?”
“Bibi Martina, sasa watu walisema yeye ni mchawi kwa hiyo
akaamua kuhamia Mbeya kwa mtoto wake Boni.”
“Sasa Iki hiyo nyumba anaishi mtu mmoja tu?”
“Hapana, Dada Asi anaishi naye, huwa anakaa pale nje na
anapenda sana kuongea na watu, kuna siku alikuja humu akaomba tumfundishe
kucheza gemu. Alisema yeye hela siyo tatizo, kuna kaka yake huwa anapita na
humpatia shilingi elfu moja kila siku.”
Nilitabasamu niliposikia jibu hili. Nilitambua wazi kuwa,
zile elfu moja ni zile ambazo nimekuwa nikimpa kila nilipopita. Kumbe
alizitumia kujifunza kucheza gemu kama alivyosema Iki. Iki hakunyamaza, raha ya
watoto wadogo hawana hofu na wakifunguka hufunguka kwa kusema yote wayajuayo.
“Ila kuna siku…” alidokeza halafu akanitazama usoni, akaona kunitazama haifai,
akainamisha kichwa chake chini. “Kuna siku mama alisema mle ndani kuna
wasichana wengi tu!”
“Kuna kingine alisema baada ya hapo?” niliuliza
nikitazama pembeni ili Iki asiniogope.
“Hapana, hata yeye hajui sana.”
Niliridhishwa na majibu ya Iki. Nikamuita kijana
aliyeshughulika na ofisi ile, nikampatia kiasi cha fedha nikimsisitiza Iki
aachwe acheze ‘game’ peke yake bila bughudha, wale wengine niliowaacha
wakipeana zamu, niliongeza malipo yao pia.
Taarifa za Iki kuwa mle ndani kulikuwa na wasichana wengi
zaidi zilinishtua. Nilipanga usiku wa siku hiyo, lazima ningeingia ndani ya ile
nyumba ili nifanye uchunguzi wa mambo mawili matatu.
Soma: Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta |Sehemu ya Saba