Mwanamke Uliyekula Pesa Zangu Nakutafuta | Sehemu ya 11
Nilikuwa barabarani natembea, ilikuwa siku ya vurugu
kwani vibanda vya wamachinga vilivyokuwa katika hifadhi ya barabara, vilikuwa
vinabomolewa na kusababisha vilio vikubwa. Inasemekana mwanzoni serikali
iliwaruhusu wafanye biashara, wakajenga vibanda, lakini sasa serikali hiyohiyo
iliwataka waondoke kwa madai kuwa ilikuwa ina wapanga vizuri. Hata sikuelewa,
nikaendelea na safari zangu.
Nilishtuka nilipopita katika nyumba aliyoishi Asi,
niligundua kuwepo kwa dalili za mtu kurejea hapo. Kwanza mazingira yalisafishwa
na taa ya nje haikuzimwa japo ilikuwa saa tisa mchana. Nikahisi kurejea kwa
Babuu. Kisha nikaandaa jambo langu.
XX XX XX
Mlango ulifunguliwa saa saba usiku, mwanamume mwenye
kipara akaingia, akabofya swichi iliyokuwa upande wa kushoto, taa ikawaka na
hapo akajionea yale asiyoyatarajia. Chumbani palikuwa na mgeni asiyekaribishwa,
tena aliikamata vyema bastola yake na alielekeza alipo, hakuonekana kuwa na
masihara hata kidogo.
Mwanamume mwenye bastola ni mimi Mako, na huyo aliyeingia
ni Babuu. Nilikaa kona ya mwisho ya kitanda, nikatengeneza umbali mzuri.
“Kaa pale,” nilimuelekeza Babuu. Naye akatii kwa kukaa
katika kiti kilichokuwa karibu na mlango. Kiti hiki kiliongezeka, mwanzoni
nilipoingia, sikukikuta.
“Wewe ni nani?” aliuliza Babuu kwa sauti nene yenye
kitetemeshi.
“Naitwa Mako,” nilijibu kwa upole.
“Sina pesa humu ndani kama ni hicho ulichofuata,”
alijitetea Babuu.
“Sijafuata pesa, shida yangu moja, niambie ulipompeleka
Asi na wenzake.”
Maneno yangu yalimshitua, hata hivyo alijikaza
akazungumza, “Wanakuhusu nini watu hao?”
“Nataka tu kujua ulipowapeleka, utaniambia au nitafute
namna ya kukulazimisha?”
Katika kosa alilofanya Babuu ni kujaribu kukimbia, muda
alipoingia, hakufunga mlango na nilimgundua muda mrefu kuwa alikuwa anapiga
hesabu za kukimbia. Hata hakuufikia mlango, nilimsindikiza kwa teke zito,
akadondoka chini kama mzigo. Sasa nikaizamisha bastola yangu katika mdomo wake.
“Utanieleza ulipompeleka Asi na wenzake?” niliuliza kwa
upole kama hakuna kilichotokea.
“Mmmmh…. Mmmhh…” alilalama bastola ikiwa mdomoni, nikaitoa
ili apate kusema.
“Asi yupo India hivi sasa, wenzake watatu wapo Misri,
wanne wapo Oman,” alijibu, nikamtazama usoni na kugundua alichosema ni kweli.
“Unafanya biashara ya kuuza watu siyo, huko India Asi
yupo mahali gani?”
“Sijui, unajua mimi kazi yangu ni kuwakusanya, kisha
anakuja ajenti mkuu, Akshay, yeye ndiyo anajua wateja, mimi napewa changu tu.”
“Sasa umejuaje kama Asi yuko India?”
“Kazi yangu nyingine ni kufuatilia hati za kusafiria kwa
kila mmoja, pia tunapoagana huwa najua kabisa huyu anakwenda huku na huyu
anakwenda kule.”
“Wakati wote ambao hukuwepo hapa, ulikuwa wapi?”
“Ajenti alikuja, hivyo tulibadili makazi na kwenda
hotelini, halafu siyo salama kukaa sehemu moja tena mwishoni mwa dili
kukamilika.”
Niliachana na Babuu, nikatoka taratibu mpaka katika
makazi yangu ambako nilipanga ramani ya kazi. Nikawa bize katika kompyuta yangu
mpakato nikituma taarifa hii na ile kuelekea nilikokujua mwenyewe.
XX XX XX
Saa tisa mchana nilianza safari kuelekea India. Dar es
Salaam nilipanda ndege ya Emirates, Boeing 777 EK 726, mimi na abiria wenzangu
tukafika Dubai saa tatu usiku, tukapata mapumziko ya saa nyingi. Saa tisa
usiku, tukapanda dege jingine la Emirates, Boeing 777 EK 510, dege hili
lilitubembeza huko angani kwa muda wa saa sita, likatushusha Delhi saa tatu
asubuhi.
Hapo New Delhi ama ninavyopenda kupaita kwa ufupisho,
Delhi, nilifikia hoteli ya bei ndogo, Airport Hotel Mayank Residency, mimi
napaita Mayank Hotel. Gharama yake ni sawa na shilingi elfu ishirini na sita tu
za Kitanzania kwa siku moja. Hii ni bei ndogo mno kwa hoteli yenye hadhi ya
nyota tatu. Tena jambo la kufurahisha ni kwamba, hotel hii ilikuwa karibu
kabisa na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Indira Ghandhi, hata wakati wa
kwenda, nilitembea kwa miguu kwani ni umbali wa kilomita moja na nusu tu. Uwanja
huu umepewa jina hili kama sehemu ya kumbukumbu ya mpigania uhuru na baba wa
taifa hilo ndugu, Indira Karamchand Mahatma Ghandi.
Chumba changu kilikuwa na kitanda kimoja cha kifahari.
Kushoto palikuwa na viti viwili na meza ndogo, na upande huohuo palikuwa na
kabati zuri lililowekwa kioo kirefu pembeni. Upande wa kulia palikuwa na
kijikabati kidogo cheusi kinacholingana na kitanda, juu yake paliwekwa simu ya
mezani.
Nilipanga kuanza msako wa Asi hapohapo Delhi. Kwa
vyovyote hakuna biashara yoyote ya maana ambayo Asi angesafirishwa kuja
kuifanya India zaidi ya ukahaba au kama angekuwa na bahati basi angefanya kazi
ya kuuza baa. Hakuna kingine cha maana ambacho angekifanya huku. Hivyo msako
wangu ulijikita katika majumba yauzayo pombe na katika madanguro.
Huu ni Mwisho wa Sehemu ya Bure ya Riwaya Hii, Isome Riwaya Yote ili Kufahamu Kilichotokea kwa Tsh. 2,000/= tu. Gusa Hapa Kununua Riwaya Yote.