Vitu Vinavyokuibia Muda Wako na kufanya Kazi Zisikamilike
Matumizi sahihi ya muda yatakufanya upate amani mahali pa kazi, uongeze ufanisi na uzalishaji. Hata hivyo, vipo vitu ambavyo vinakuibia muda wako na kukufanya uone siku haitoshi ilhali saa ni nyingi. Unapenda kuvifahamu vitu vinavyokuibia muda wako? Soma taratibu.
1. Simu
Simu ni mwizi wa kwanza wa muda. Wakati wa kazi, unaweza kupigiwa simu ukapokea na kuongea kwa zaidi ya dakika ishirini. Utajibu meseji kadhaa, utaingia katika mitandao ya kijamii kutazama habari mbalimbali, ukija kukaa sawa ili ukamilishe kazi, muda umekwisha!
2. Kelele
Wapo watu wanaofanya kazi katika mazingira yenye kelele nyingi. Kelele hupunguza ufanisi kwani mtu hushindwa kufikiri haraka ili kukamilisha jambo. Fikiria mtu anayefanya kazi katika mazingira ya kelele, anaamua kutafuta sehemu yenye utulivu ili atume au asikilize taarifa fulani muhimu, hatua zote hizi zinapoteza muda.
3. Vikao
Vikao vya ofisi navyo ni sehemu ya wezi wa muda. Vikao vingi huwa havina jambo la maana zaidi ya kukumbushana mambo yaleyale ya kila siku. Haimaanishi kwamba vikao visiwepo kabisa, lakini ofisi ijitahidi kuitisha vikao vyenye tija na muda uliopangwa ufuatwe.
4. Runinga
Runinga inapoteza muda wako. Unaweza kusitisha kazi fulani, ili utazame tamthiliya fulani kisha utaendelea. Matokeo yake muda mwingi unatumika katika kutazama runinga hivyo kazi hazikamiliki kwa wakati. Hata hivyo kupumzika na kuangalia runinga siyo kosa, lakini ifanyike katika namna ambayo haitapoteza muda wa kazi.
5. Wewe mwenyewe
Ndiyo, wewe ni mwizi wa muda wako. Ni mwizi wa muda wako kwa sababu unafanya mambo bila mpangilio. Unajifanyia tu bila kujali kipi muhimu na kipi si muhimu. Unapofanya kazi, hakikisha unaorodhesha mambo yote unayotaka kuyafanya katika siku hiyo. Kisha anza kufanya kazi ukizingatia lipi muhimu nalipi si muhimu sana.
6. Marafiki
Marafiki ni wezi wa muda wako. Rafikia anaweza kukuomba umpeleke sehemu fulani, au pengine akakupigia simu wakati wa kazi. Akakutembelea wakati wa kazi na ikafaa kumjali zaidi na kuahidi kufanya kazi baadae. Hatupaswi kukosa marafiki, lakini tutenge muda wa kazi na ule wa marafiki.
7. Mambo mengi kwa wakati mmoja
Wapo watu wanaofanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kujikuta wakishindwa kukamilisha hata jambo moja. Nitatoa mfano wa mwalimu anayesahihisha mtihani, lakini muda huohuo anatazama runinga, muda huo anajibu meseji na muda huohuo anajadiliana na wenzake kuhusiana na mechi fulani. Kwa Hakika hakuna kazi itakayokamilika hapo.
Hayo ni baadhi ya mambo yanayoiba muda wako. Ni vyema basi kuwa makini na mambo haya ili tuweze kuongeza ufanisi mahali pa kazi.
Mambo ya kuzingatia ili kuepuka kupoteza muda
1. Kataa vikao visivyo na manufaa kwako na visivyo vya lazima kuhudhuria. Unapokubali kwenda katika vikao, hakikisha muda uliopangwa unatumika na si zaidi yake.
2. Weka orodha ya mambo yote unayotaka kuyakamilisha katika siku fulani. Tengeneza tabia ya kuandika mambo unayotaka kuyakamilisha kila siku.
3. Pumzika, usikae muda mrefu katika kiti. Pumzika kidogo mwili upate nguvu. kwa anayetumia kompyuta, anashauriwa kupumzika kila baada ya dakika ishirini. Simama, jinyooshe, tembea kidogo, rudi endelea na kazi.
4. Zuia usumbufu. Wafahamishe watu hutaki kusumbuliwa unapokuwa unafanya kazi.
5. Pata muda wa kulala. Kukosa usingizi au kushindwa kulala kwa muda unaofaa kutakufanya ushindwe kufanya kazi zako vizuri. Hakikisha unalala mapema na unaamka mapema. Hakikisha unapata angalau saa nane za kulala. Haiwezekani? Basi saa saba. Nazo haziwezekani, fanya sita. Pata saa nyingi za kulala ili akili ipate pumziko na iweze kufanya kazi siku inayofuata.
Ukizingatia hayo, utafaidika katika kazi zako. Kukamilisha kazi kutakupunguzia msongo wa mawazo. Ni wakati sasa wa kuwaepuka wezi wa muda kwa kuzingatia mambo yaliyoelekezwa.