Utungaji wa Kazi za Fasihi Andishi | Kiswahili Kidato cha 3

Mkono unaandika katika karatasi nyeupe.

Utungaji ni namna au jinsi ya kupangilia visa na matukio katika maandishi kwa lengo la kuburudisha, kuelimisha na kuakisi hali ya maisha ya jamii inayohusika.

Hadithi fupi

Hadithi fupi ni masimulizi ya kubuni yanayosawiri tukio, tabia, mgogoro au kipengele cha maisha.

Hadithi fupi huwa na tukio moja au mawili na hutumia mawanda finyu.

Hadithi fupi huwa na wahusika wachache na huandikwa kwa muda mfupi.

Baadhi ya fani zilizochangia kuibuka kwa hadithi fupi ni: ngano, hekaya, visasili, michapo na tendi.

Katika kutunga hadithi fupi, sharti upendekeze visa vya kutungia. Mfano wa visa hivyo ni kisa cha jogoo kuwa na kishungi au kisa cha twiga kuwa na shingo ndefu.

Mfano wa hadithi fupi

PURUKUSHANI USIKU WA MANANE

Ilikuwa usiku wa siku ya Jumatano, Mowasha alijilaza katika kitanda chake cha teremka tukaze kwa furaha kuu. Ajabu ni kwamba hakukumbuka hata kuvua viatu, alilala navyo!

Kilichompa furaha Mowasha hakikuwa kitu kingine bali fedha aliyoipata baada ya kuuza pamba yake, pamba aliyohangaika kuilima leo ilimpa mamilioni, kweli mchumia juani hulia kivulini.

Akiwa amelala tena hajitambui kwa sababu ya usingizi, ghafla alistushwa kwa kupigwa kofi zito la mgongo, kofi hilo lilimpa simanzi na kumfanya alie kwa maumivu.

“Toa fedha uishi.” Jambazi mmoja alimwamulisha Mowasha, Mowasha akamtazama bwana huyu usoni akagundua ya kuwa jambazi huyu alikuwa mweusi kama kipande cha giza!

Jambazi yule aliendelea kumchapa makofi mazito ya uso Mowasha, kuna wakati jambazi alisikika akisema, “Toa fedha niko kazini!”

Mowasha baada ya kuona anaweza kufa, akainama chini ya mvungu wa kitanda chake akatoa kitita kikubwa cha fedha, jambazi bila kupewa fedha zile akazikwapua na kutokomea kusikojulikana.

Mowasha alihuzunika sana baada ya kuibwa fedha zake, alionekana mnyonge kama mtoto wa panya aliyekutana na paka mkubwa, lakini hakukata tamaa, aliendelea na shughuli za kilimo, safari hii hakulima pamba peke yake, alilima machungwa, nyanya na matikiti. Hivi sasa anamiliki nyumba mbili za ghorofa.

Utungaji wa riwaya

Riwaya ni hadithi ndefu ya kubuni yenye mawanda mapana, lugha ya kinathari, mchangamano wa visa, dhamira, wahusika wengi na matukio yaliyosukwa kimantiki.

Riwaya inaweza kwa ya masimulizi ya kweli au ya kubuni.

Mfano wa riwaya za Kiswahili ni: Joka la mdimu, Watoto wa Mama Ntilie na Takadini.

Mikondo ya riwaya

1. Mkondo wa kiwasifu

Huhusu hadithi zinazosimulia maisha ya watu au mtu kutoka kuzaliwa kwake hadi wakati anapoandika riwaya hiyo. Mfano wa riwaya ya Kiwasifu ni Wasifu wa Sitti binti Saad.

2. Mkondo wa kitawasifu

Husimulia maisha ya mtu binafsi yaani mwandishi mwenyewe. Mfano wa riwaya ya kitawasifu ni Maisha yangu na baada ya miaka Hamsini.

3. Mkondo wa kipelelezi

Huzungumzia upelelezi wa uhalifu fulani kama vile ujambazi, wizi, rushwa na mauaji. Mfano ni riwaya ya Njama.

4. Mkondo wa kihistoria

Huhusu matukio yua kweli ya kihistoria yaliyowahi kutokea. Mfano riwaya ya Zawadi ya ushindi.

5. Mkondo wa kijasusi

Huhusu hadithi ya upelelezi wa ngazi ya kimataifa. Mfano wa riwaya ya kijasusi ni riwaya ya Njama.

6. Mkondo wa kimapenzi

Huzungumzia masuala ya mapenzi ya wazi kati ya mwanamke na mwanaume. Mfano wa riwaya ya mkondo wa kimapenzi ni Rosa Mistika.

Mfano wa riwaya

Bwana Mako alinyanyuka katika sofa, akarusha mateke na ngumi mfululizo mpaka alipohisi yupo sawa kwa mapambano. Mwenye uchungu na nchi yake, alikisogeza pembeni kitanda, kisha akafunua chini katika sakafu, humo alificha siraha zake nyingi za maangamizi. Aliamua kuchukua siraha mojawapo, bunduki ya kisasa, Norinco 97, akaifuta vumbi na kuirudisha pahala pake. Alipomaliza ukaguzi wa siraha, akapanga kila kitu kama kilivyokuwa awali, kisha akachukua simu yake na kumwandikia ujumbe mfupi Lightness, “kazi imeanza.”

Nchi ya Andalasu ilikuwa katika shida kubwa. Mgodi pekee uliotegemewa na taifa hili masikini, ulivamiwa na kundi la wanyang’anyi waliokuwa na siraha za moto. Haikufahamika ni nani alikuwa nyuma ya kundi hili. Kwa kuwa mgodi huu unaotoa almasi kwa wingi kuliko mgodi wowote ule Duniani ulikuwa mikononi mwa wanyang’anyi, serikali ilipoteza fedha nyingi na ilianza kushindwa kujiendesha, hali ilikuwa mbaya katika serikali na uchumi wa nchi nzima.

Mgodi ulipotekwa mara ya kwanza, kilitumwa kikosi cha askari kwenda kuukomboa, askari wote waliuawa. Baada ya hapo kikatumwa kikosi cha makomandoo, ambacho nacho kilifyekelewa mbali na hakuna aliyebaki. Vikosi vingi viliendelea kutumwa na matokeo yalikuwa yaleyale, hakuna aliyerudi akiwa hai. Serikali ikawa katika hofu kubwa ya wanyang’anyi hawa wasiofahamika.

Vikosi vingine vilipotumwa kwenda kupambana na wanyang’anyi hawa, vilikataa kwa kutoa sababu kuwa, silaha walizotumia wao zilikuwa za kiwango cha chini mno ukilinganisha na wanyang’anyi ambao wao walitumia silaha kali zaidi. Wakati askari wa serikali wakienda kuvamia wakiwa na siraha aina ya SMG yenye uwezo wa kubeba risasi 30, wanyang’anyi walitumia siraha za maangamizi kama IWI X95 TAVOR ambayo iliweza kupiga risasi 950 kwa dakika, mbali na hayo, walikuwa na makombora aina ya FIM 92, yaliyokuwa na uwezo kusabaratisha ndege na vifaru! Mwenye nguvu mpishe!

Utungaji wa tamthiliya

Tamthiliya ni mchezo wa kuigiza ulioandikwa ili utendwe jukwaani au usomwe kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii.

Sifa za tamthiliya

I. Kusudi maalumu

II. Waigizaji

III. Jukwaa au mahali pa kuigizia

IV. Watazamaji (hadhira)

V. Ubunifu

VI. Mpangilio wa matukio

VII. Mtindo wa majibizano

VIII. Dhana inayotendeka

Dhima za tamthiliya

I. Kuelimisha.

II. Kuburudisha.

III. Kusisimua.

IV. Kuonya na kuadabisha.

V. Kuhamasisha shughuli za kimaendeleo.

VI. Kutunza kumbukumbu (amali) za jamii.

Mambo anayopaswa kuzingatia mtunzi wa tamthiliya

I. Kuchagua jambo au kisa anachotaka kuandika.

II. Kupanga visa namatukio.

III. Kubuni wahusika sahihi.

IV. Kuchagua mandhari inayofaa.

V. Kugawa matukio.

VI. Kutoa maelekezo ya jukwaa kwa kila kipande cha maonesho.

Tanzu za tamthiliya

1. Tanzia

Ni tanzu ya tamthiliya ambayo husikitisha na kuhudhunisha na hugusa hisia za hadhira.

Hadhira inayoangalia huweza kuogopeshwa na kumwonea huruma mhusika mkuu ambaye mwishowe huishia kupata janga.

Mhusika mkuu huwa na tabia njema na msimamo na jamii humkubali.

Mfano wa tamthiliya ya Tanzia ni: Orodha, Kilio chetu na Mfalme Edipode.

2. Ramsa

Ni tanzu ya tamthiliya ambayo visa na matukio hujengwa katika kuchekesha na kufurahisha.

Visa vyake hujikita katika maisha na uwepo wa kifo.

Mhusika mkuu hutumia njia rahisi katika kukabiliana na maisha bila kujali njia itakayotumika ni halali au siyo halali.

Mara nyingi ramsa hailaani uovu bali hukejeli ujinga wa binadamu na haioni huruma kwa wahusika wake wanapoumbuka au kuaibika.

Mwisho wahusika wakuu huibuka na mafanikio.

Mfano wa tamthiliya aina ya ramsa ni: Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe, na Mfalme Juha.

Mfano wa tamthiliya

Vitumbua Vitamu

ONYESHO LA KWANZA

(Jukwaani wanatokea Kipisi na Mwantumu, Kipisi anatembea haraka na kumkamata mkono Mwantumu)

Kipisi: Habari yako sista…

Mwantumu: salama karibu biashara. (Anashusha chini sufuria lililojaa vitumbua, Kipisi anachukua vitumbua viwili na kuanza kutafuna)

Kipisi: Asante sista, nimetafuna viwili, vitumbua vitamu sana. Kwa heri!!

Mwantumu: Kwa heri hiyo vepee? Nilipe fyeza yangu, shilingi mia mbili.

Kipisi: sikulipi, fanya unachoweza.

Mwantumu: ahaa… kwa kuwa mi mwanamke ndo unanichukulia poa sio? Sasa leo nitakuonesha utamu wa mihogo pilipili.

(Mwantumu anamkunja shati Kipisi, kisha anampiga mweleka na kumfanya kipisi adondoke chini kama gogo.)

Kipisi: we mwanamke nuksi, chukua pesa yako usije niua bure.

Zingatia kuwa swali liulizwapo, huelezea urefu unaotakiwa katika hiyo tamthiliya yako.

Zoezi la marudio

2. Chagua jibu sahihi katika maswali yafuatayo:

i. Hadithi inayokuwa na wahusika wachache huitwa:

A. Riwaya

B. Tungo

C. Hadithi fupi

D. Kisa

E. Utenzi

ii. Tamthiliya ambayo mwishoni wahusika wake wakuu huonesha kufanikiwa inaitwa:

A. Tanzia

B. Ramsa

C. Kilio chetu

D. Ngoswe

E. Mikondo

iii. Tamthiliya ipi huambatana na masikitiko pamoja na huruma?

A. Vichekesho

B. Ramsa

C. Ngoswe

D. Tanzia

E. Mfalme Juha

iv. Riwaya ambazo husimulia maisha ya mtu binafsi huwa katika mkondo upi?

A. Kihistoria

B. Kimapenzi

C. Kitawasifu

D. Kiwasifu

E. Kimaadili

2. oanisha maelezo ya orodha A na maneno yake katika orodha B

Orodha A

I. Kupangilia visa na matukio katika maandishi kwa lengo la kuburudisha, kuelimisha, na kuakisi hali halisi ya jamii.

II. Masimulizi ya kubuni yanayosawiri tukio, tabia na migogoro katika maisha.

III. Mambo ya kubuni yenye mawanda mapana, lugha ya kinathari, mchanganuo wa visa, dhamira na wahusika kadhaa.

IV. Mchezo wa kuigiza unaoandikwa ili utende jukwaani.

Orodha B

A. Riwaya

B. Utungaji

C. Tamthilya

D. Hadithi

E. Visa

F. Masimulizi

3. Je, unafikiri ni changamoto zipi atakazokutana nazo mwandishi endapo hatakuwa na mzawa wa eneo hilo?

4. Eleza sababu za mtunzi kuelewa jamii kabla ya kuiandikia kazi ya fasihi.

5. Andika hadithi fupi kuhusu dhima za fasihi andishi.

6. Eleza mambo ya kuzingatia katika utunzi wa riwaya.

7. Eleza mambo ya kuzingatia katika utunzi wa tmthiliya.

8. Onesha uhusiano uliopo baina ya utunzi wa riwaya na tamthiliya.

9. Kuna tofauti gani kati ya utunzi wa riwaya na tamthiliya?

10. Tamthiliya yenye kusikitisha inaitwaje?

Marejeo:

Makoba, D. (2017) “Jinsi ya kujibu maswali ya kiswahili katika mtihani wa taifa - swali la 15”. Inapatikana katika https://www.mwalimumakoba.co.tz/2017/04/jinsi-ya-kujibu-maswali-ya-kiswahili.html. Ilisomwa tarehe 01 Oktoba 2024.

TET. (2021) Kiswahili Kidato cha Tatu. Dar es Salaam: Taasisi ya Elimu Tanzania.

Popular posts from this blog

Jinsi ya Kuandika CV | Mfano wa CV Wasifu

Fasihi ni Zao la Jamii | Harusi ya Dogoli na Vuta n’kuvute

Jinsi ya Kuandika Barua ya Maombi ya Kazi Mwaka 2024